

Lugha Nyingine
新年大战 每日壕送2万元
![]() |
Mwanasarakasi wa Kenya Mathias Kavita (wa kwanza, kulia) akimwelekeza mtoto kucheza sarakasi mjini Thika, Kenya, Julai 11, 2025 (Xinhua/Han Xu) |
NAIROBI - Huku zaidi ya vijana 1,000 wakiwa wamepitia mafunzo yake, mwanasarakasi Mkenya Mathias Kavita alikuwa amejawa fahari wakati akikumbuka uhusiano wake wa miaka 41 na China, ambao umevuka wakati na jiografia kustawi wakati akifanyiwa mahojiano ya hivi karibuni na Shirika la Habari la China, Xinhua.
Muda mfupi kabla ya siku yake ya kuzaliwa kutimiza miaka 12 mwaka 1983, safari ya Kavita kwenda China kujifunza sarakasi chini ya udhamini wa serikali iliashiria mabadiliko katika maisha yake, ikimwelekeza kwenye ulimwengu mpya wa kijasiri wa michangamano ya tamaduni mbalimbali na urafiki wa kudumu.
Kwa miaka miwili, Kavita na wenzake 23 waliishi katika Kikundi cha Sarakasi cha Guangzhou, katika Mkoa wa Guangdong, kusini mwa China ambapo walipitia mafunzo makali, ikihitimisha kwa wao kupata umahiri wa mchezo huo.
Muda mfupi baada ya kukamilisha programu hiyo, Kavita alirudi nyumbani kwao, alifanya kazi kama mkufunzi wa sarakasi katika kampuni binafsi, na baadaye akaanzisha kampuni yake katikati ya miaka ya 1990 ili kulea na kukuza kizazi cha siku za baadaye cha wanasarakasi.
Katika jamii moja katika mji wa viwanda wa Thika katikati mwa Kenya, kocha huyo mchangamfu wa sarakasi alikuwa katika kituo chake alipokusanya kundi la watoto kwa ajili ya mafunzo ya saa moja, yaliyoshirikisha kuruka na kupanda kamba.
"Nimekuwa katika nyanja hii tangu nilipofundishwa sarakasi na Wachina," amesema Kavita, akiwa amevalia viatu vyeusi vya jadi vya Kichina vyenye soli laini, ambavyo kwa kawaida huvaliwa na wazee katika nchi hiyo ya Asia. Wasaidizi wake wawili wa kiume walikuwa wamevalia sare zilizoandikwa "Hebei Wuqiao Acrobatic Art School."
Julai 2024, Kavita alitembelea Wilaya ya Wuqiao, iliyoko Mkoa wa Hebei, kaskazini mwa China, kushiriki katika programu ya miezi miwili ya mafunzo na mawasiliano ya ujuzi wa sarakasi, inayofadhiliwa na serikali ya China.
"Wakati nilipokanyaga ardhi hii baada ya miaka 41, kiukweli nilihisi kama nimerejea nyumbani. Kwa zaidi ya miaka 40, nimekuwa nikidumisha kwa thamani kumbukumbu zangu za China," Kavita amesema.
Kavita amehifadhi "hazina iliyofichwa" ya kumbukumbu kutoka kwenye uhusiano wake na China, ikiwemo cheti cha kuhitimu kutoka Kundi la Sarakasi la Guangzhou, visa kutoka safari yake ya kwanza kwa China, na picha za kundi zilizopigwa wakati wa vipindi vilivyopita vya mafunzo.
Mwezi Juni, Kenya iliadhimisha miaka 40 ya mawasiliano na ushirikiano wa kitamaduni wa sarakasi na China katika hafla ya gala ambapo Kavita aliongoza vijana kuonyesha umahiri wao katika mchezo huo.
Kwa miaka mingi, Kavita anaona kwamba umaarufu wa sarakasi nchini Kenya umeongezeka kwa kiasi kikubwa, ukichochewa na watoto na vijana wanaotaka kuongeza kwa kina uelewa wao wa utamaduni wa Kichina.
"Sarakasi imepitia hali mbalimbali tangu niliporudi kutoka China miaka 40 iliyopita. Kile nilichojifunza mwaka jana nchini China ndicho ninachotaka kutekeleza katika mafunzo yetu ya sarakasi hapa Kenya," amesema.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma